IQNA

Maulidi

Wapalestina  wasoma Qur'ani katika katika sherehe za Maulidi  katika Masjid Ibrahmi

17:22 - September 16, 2024
Habari ID: 3479444
IQNA – Hafla maalumu ya kusoma Qur'ani ilifanyika mjini Al-Khalil katika Masjid Ibrahimi kwa mnasaba wa Milad-un-Nabi au Maulidi ambayo ni maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Halqa hiyo  iliandaliwa katika msikiti wa Masjid Ibrahim siku ya Jumapili ambapo wahifadhi Qur'ani 1,300 wa kiume na wa kike walisoma  Surah Al-Baqarah, ambayo ni sura ndefu zaidi ya Qur'ani

Sheikh Mutaz Abu Sneina, mkurugenzi wa Masjid Ibrahimi, alisema hafla hiyo ya Maulidi ilihudhuriwa na idadi kubwa ya waumini na kuongeza kwamba ilifanyika chini ya usimamizi wa Idara ya Wakfu ya Al-Khalil, alisema.

Tukio hilo la Qur'ani Tukufu lilikuwa ni sehemu ya juhudi zinazolenga kuimarisha uwepo wa waumini wa Kiislamu katika Msikiti wa Ibrahimi, ambao umekuwa ukinajisiwa na wanajeshi na walowezi wa utawala wa Kizayuni Israel mara kwa mara, alisema.

Msikiti wa Ibrahimi uligawanywa na kuwa sinagogi, linalojulikana kwa Wayahudi kama Pango la Mababu, na msikiti baada ya mlowezi wa Kiisraeli mzaliwa wa Marekani Baruch Goldstein kuwaua Wapalestina 29 ndani ya msikiti huo mwaka 1994. Tangu wakati huo, waumini wa Kiislamu wamezuiwa kuingia katika msikiti huo wakati hafla za Kiyahudi.

Baada ya Israel kuuteka Ukingo wa Magharibi mwaka 1967, iligawanya al-Khalil katika miji tofauti ya Waislamu na Wayahudi.

Al-Khalil, mji ambao Wayahudi wanauita Hebron, ndio mji mkubwa zaidi katika Ukingo wa Magharibi, wenye Wapalestina zaidi ya 200,000. Walowezi wapatao 1,000 wa Israel, ambao wanafanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Wapalestina, pia wanaishi humo chini ya ulinzi mkali wa jeshi katili la Israel.

Ikumbukwe kuwa siku kama ya leo miaka 1499 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Mas'udi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW.

Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani.

Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.   

3489918 

Habari zinazohusiana
captcha